Monday, June 29, 2020

Watano mbaroni na vyeti feki 90 vya uuguzi

POLISI mkoani Kigoma imewatia mbaroni watu watano akiwemo askari mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za kutengeneza vyeti bandia vya kitaaluma, miongoni mwake vikiwemo 90 vya uuguzi, ambavyo vilikutwa vikisubiri kugawiwa kwa wahusika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema kuwa pamoja na vyeti hivyo vya uuguzi vilivyokamatwa, pia katika operesheni hiyo walikamata vyeti 37 vya wataalamu wa maabara na vyeti tisa vya ufamasia.

Alisema kuwa katika operesheni hiyo iliyofanywa kwa pamoja na maofisa kutoka Baraza la Wafamasia nchini, walikamata jumla ya vyeti 936 vikiwa kwenye hatua ya ukamilishaji vikiwa bado havijaandikwa majina, miongoni mwake vikiwemo vyeti 667 vya wauguzi wasaidizi, vyeti 126 vya wataalam wa maabara, cheti kimoja cha mafunzo ya afya ya jamii na vyeti viwili vya utoaji huduma ya kwanza.

Katika kuhakikisha wanakuwa na uthibitisho wa tuhuma hizo, Kamanda Mtui alisema kuwa pia wamekamata mihuri 25 ya taasisi mbalimbali ikiwemo nyundo mbili, ambazo hutumika kutengenezea mihuri mbalimbali ya moto.

Aliwataja watu waliokamatwa katika operesheni hiyo ambayo inahusisha mtandao wa watu mbalimbali kuwa ni askari wa JWTZ, Mgeni Nyamubozi ambaye ni mume wa mmiliki wa Duka la Vifaa vya Ofisi la Upendo, lililopo Mwanga mjini Kigoma, ambalo linatuhumiwa kuhusika na utengenezaji wa vyeti hivyo.

Katika duka hilo, Kamanda huyo wa polisi alisema polisi walikamata kompyuta mpakato moja, ikiwa na nakala za vyeti mbalimbali za vyuo na idara za serikali.

Mwingine aliyekamatwa ni Dickson Mshahili, muuguzi katika Hospitali ya Mkoa Kigoma ambaye katika upekuzi nyumbani kwake, alikutwa na nyaraka mbalimbali ikiwemo madaftari 12 yakiwa na kumbukumbu za vyeti anavyotengeneza na mihuri ya waganga wakuu wa mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Singida na Tabora.

Sambamba nao alikamatwa Zawadi James, muuguzi wa Kituo cha Afya Ujiji ambaye baada ya kupekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na vyeti vitatu na kabuleta ya pikipiki ambayo hutumika kutengeneza mihuri ya moto.

Wengine waliokamatwa ni Johnson Nyabuzoka, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole ya mjini Kigoma, ambaye ni mtaalam wa kompyuta aliyekuwa akitumika kufanya kazi hiyo; na Stephano Erasto ambaye alikamatwa katika siku yake ya kwanza tangu ajiunge na duka hilo kwa ajili ya kusaidia kazi.

CHADEMA: Mbowe anaendelea vizuri ila anakandamizwa

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa CHADEMA Tumaini Makene, amesema kuwa licha ya kwamba Mwenyekiti wa chama hicho kushambuliwa na kuumizwa lakini bado ameendelea kukandamizwa kutokana na baadhi ya taarifa ambazo zinatolewa kuwa ni za makisio na si zile zinazotokana na uchunguzi.

Makene amesema hali ya Mbowe kwa sasa anaendelea vizuri, lakini wamekuwa wakishangazwa na matokeo ya uchunguzi uliotolewa, huku wakidai kuwa na mashaka kwani uchunguzi hauko huru wala wazi.

"Bahati mbaya kila ukisikia kauli za Polisi bado wanaonekana wameshatengeneza points za kumshambulia na kumkandamiza muathirika wa tukio la kuvamiwa na kushambuliwa, na wanakuwa wako 'very bias' tunakosa hata uchunguzi wa uhuru unaofanywa na Polisi badala ya kujielekeza kupata ukweli wa tukio ili mwisho wa siku kukomesha vitendo hivi" amesema Makene.

Mbowe alishambuliwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Juni 9, 2020, wakati akipandisha ngazi kuelekea nyumbani kwake Jijini Dodoma, ambapo baadaye taarifa ya Polisi ilitolewa na kuonesha kuwa siku ya tukio Mbowe alikuwa amelewa chakari.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa wafuasi watano wa Chadema

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa wafuasi watano wa Chadema  wanaokabiliwa na kesi ya jinai yenye mashitaka saba mahakamani hapo  baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Katika kesi hiyo, viongozi na wafuasi 27 wa Chadema wanakabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kukaidi amri halali na kuharibu geti la gereza la Segerea.

Washitakiwa hao ambao  hawajafika na kuamriwa kukamatwa ni Edga Adelin, Gerva Yenda, Regnald Masawe, Cesilia Michaeli na Paulo Makali.

Mapema, wakili wa Serikali Ester Martin alidai mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi,kuwa kesi hiyo leo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali lakini upande wa mashtaka haujajiandaa hata hivyo washtakiwa wengine hawapo.

Kufuatia m111¹qaelezo hayo Hakimu Shahidi aliuliza kama wadhamini wa washtakiwa wapo ili kueleza sababu za washtakiwa hao kutokufika Mahakamani hata hivyo hakuna mdhamini aliekuwepo.

Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, mwaka huu kwa ajli ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Washitakiwa wengine  katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa baraza la wananwake (bawacha) Halima Mdee, aliyekuwa mnadhimu wa kambi ya upinzani Ester Bulaya,  Mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida Jesca Kishoa, aliyekuwa Meya wa Ubungo Boniface Jacob, Diwani wa Tabata Patrick Assenga na Mshewa Karua.

Wengine ni  Khadija Mwago, Pendo Mwasomola, , Happy Abdallah, Stephen Kitomali,Athumani Hassan, Omary Milodo, Emmanuel Ignastemu, Stephen Kitomali, Hamis Yusuph, Juma Juma, Mustafa Lada, Emmanuel Zakaria na Steven Ezekiel.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Machi 13, 2020 washitakiwa hao wakiwa katika gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, isivyo halali na kwa makusudi walikaidi amri iliyotolewa na askari B 3648 SGT John ambaye  aliwataka wahusika hao kuondoka eneo hilo la magereza na alikuwa akitimiza wajibu wake aliyopewa.

Mashtaka mengine ni kukusanyika eneo la Magereza isivyo halali na kupelekea kuleta hofu na kuhatarisha amani na utulivu kwenye eneo hilo,kufanya uharibifu wa geti la Segerea ambalo ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mashtaka mengine ni kutoa lugha ya kuudhi ambalo linalomkabili Mdee na Bulaya ambapo inadaiwa siku hiyo walitoa maneno ya kuudhi kwa askari magereza Sajenti B 3648 John, maneno ambayo yalipelekea uvunjifu wa amani.

Pia inadaiwa katika tarehe hiyo mshitakiwa Jacob akiwa eneo la gereza la Segerea alitamka maneno ya kuudhi kwa Sajenti B 3648 John na kufanya shambulio kwa askari magereza huyo kwa kumkunja na kumvuta shati wakati akitekeleza majukumu yake.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini SACP David Misime imesema kuwa……..

Leo 24/06/2020 Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amefanya uhamisho kwa baadhi ya Makamanda wa Polisi wa mikoa ili kuongeza ufanisi na tija katika kazi za Polisi. Miongoni mwa waliohamishwa, amemhamisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Salum Hamduni kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha na aliyekuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Jonathan Shana amehamishwa kwenda kuwa Afisa Mnadhimu namba moja  katika Shule ya Polisi Moshi.

Pia IGP Sirro, amemhamisha aliyekuwa Afisa Mnadhimu Bunge, Dodoma ACP Emmanuel Lukula kwenda kuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro na nafasi yake inachukuliwa na ACP Andrew Satta ambaye alikuwa Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Polisi Dodoma.